Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali kupitia mradi wa kuendeleza elimu ya Juu tayari imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Buyu, Zanzibar.
Akizungumza baada ya kukagua chuo hicho Waziri Ndalichako, amesema mbali ya fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo.
“Mbali ya kutenga fedha za ujenzi wa mabweni, lakini mimi na Katibu Mkuu tulishaanza kufanya mapitio miradi tuliyonayo katika wizara kuona inawezaje kusaidia kukamilisha ujenzi wa majengo yote yaliyoishia katika hatua ya msingi ambayo ni muhimu katika kukamilisha mafunzo,” Amesema Profesa Ndalichako.
Aidha Waziri Ndalichako amesema kuwa serikali haitokaa kimya endapo itaona fedha hizo zinapotea bila kukamilisha ujenzi, kwani matamanio ya serikali ni kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.
Sambamba na hayo Waziri Ndalichako ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kuanza masomo bila kuogopa changamoto walizonazo. Amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan juu ya kuandaa vijana wenye ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.