Serikali ya Tanzania ipo mbioni kuanza kuwachukulia hatua wanaosambaza katika mitandao ya kijamii taarifa za uongo kuhusu madhara anayoweza kuyapata mtu iwapo atatumia aina flani ya dawa.
Hayo yamesemwa hii leo Alhamisi Agosti 29, 2019 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea Ofisi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) akiongozana na kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Amesema kuwa dawa zinazouzwa nchini huthibitishwa ubora wake na TMDA kabla ya kuuzwa na hakuna dawa iliyo bora zaidi ya nyingine.
”Niwaombe wananchi kutosambaza taarifa ambazo hawana uhakika nazo, kama wana swali au hoja kuhusu ubora wa dawa ni bora wawasiliane na TMDA kwa sababu sasa tutaanza kuchukulia hatua kwa upotoshaji usio na msingi,” amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha, amesema kuwa wananchi hawapaswi kuwa na mashaka na dawa zinazouzwa katika maduka kwasababu maabara ya TMDA inaongoza kwa ubora Barani Afrika na wapo katika mkakati wa kuomba kibali cha kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Tukipata kibali majibu ya vipimo tutakayokuwa tunayatoa Tanzania yatakuwa yanakubalika dunia nzima na itakuwa ni hatua kubwa kwetu,” amesema Dkt. Ndugulile.