Waziri wa Habari, Utamadani, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewahakikishia wadau wa sekta ya utangazaji nchini ikiwemo waandaaji na wazalishaji wa vipindi vya televisheni vya maudhui ya ndani kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao na kuwajengea mazingira wezeshi ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao.
Akizungumza katika kikao maalum baina yake watayarishaji wa vipindi vya maudhui ya ndani jana Alhamisi (Julai 25, 2019) Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa tasnia ya habari inapiga hatua kubwa za maendeleo.
Waziri Mwakyembe alisema Serikali inatambua wajibu na umuhimu wa tasnia ya habari nchini, na hivyo imetunga sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza vyombo vya habari ikiwemo televisheni, ambapo vimewekewa utaratibu wa kurusha na kuandaa vipindi mbalimbali kupitia miongozo inayotolewa mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Tunatambua kuwa kuna baadhi ya vifungu vya kisheria vinavyoongoza maudhui ya vituo vya utangazaji vimekuwa changamoto, kwa kuwa Sheria hizi sio biblia au msahafu takatifu, tunaweza kuzifanyia marekebisho kila baada ya kipindi cha miaka 3-4 ili kuona ni namna gani inasaidia sekta ya utangazaji sambamba na kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza,”amesema Waziri Mwakyembe.
Aidha, Waziri Mwakyembe amesema kuwa wizara yake ipo tayari kupokea aina yoyote ya ushauri, mapendekezo na maoni ya wadau wa wazalishaji na waandaaji wa vipindi vya Televisheni hususani masuala yote ambayo yamekuwa yakiwaletea changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matukio wa Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) Martha Swai amesema TBC imekuwa mstari wa mbele katika kutangaza vipindi vyake vya Televisheni katika maudhui ya ndani, ambapo asilimia 82 vimegusa masuala ya elimu, biashara na kuburudisha, na asilimia 18 ikijikita katika masuala ya muziki.
Naye Meneja Vipindi wa Kampuni ya Tumaini Media, Paul Mabuga amesema kwasasa kumekuwepo na changamoto kubwa ya ukosefu wa matangazo ya biashara katika vituo vya Televisheni kwani wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia zaidi mitandao ya kijamii ili kuweza kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa njia ya kisasa na haraka zaidi.