Serikali nchini, imesema itaendelea kuboresha uwezo wa kupambana na majanga kwa kuimarisha sheria za mifumo ya kitaasisi na kutoa mafunzo ya pamoja miongozi mwa vyombo ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Novemba 3, 2022 Bungeni jijini Dodoma, na kuongeza kuwa wakati wote pia Serikali itahakikisha upatikanaji wa vifaa vya tahadhari, uokozi na kutoa huduma mapema kwa waathirika unakuwa ni wa uhakika.
Majaliwa ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki na kuzuka kwa moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Waziri Mkuu, pia ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mkoa wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Ameendelea kutoa shukrani pia kwa Majeshi, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA), taasisi mbalimbali za Kiseerikali na zisizo za Serikali, wananchi wa vijiji vya jirani na hifadhi pamoja na wadau wote walioshiriki kikamilifu katika uzimaji wa moto uliozuka katika mlima Kilimanjaro.