Serikali nchini, imesitisha kwa muda wa miezi mitatu zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki, wakati ikiendelea na tathmini ambayo itawezesha kutoa muongozo wa namna bora zaidi ya utekelezaji zoezi hilo.

Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hii leo Novemba 3, 2022 Bungeni jijini Dodoma, na kusema bei elekezi ya kuweka hereni za kielektroniki kwa mnyama mmoja ni shilingi 1,750 kwa ng’ombe, shilingi 1,000 kwa Punda, mbuzi na kondoo ambapo gharama hizo zimekuwa zikilalamikiwa na wafugaji kwamba ni kubwa tofauti na uhalisia.’

Zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki.

Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki na kuzuka kwa moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Waziri Mkuu amesema, ’’Serikali imesikia hoja za wafugaji kuhusu mapungufu ya kanuni, usimamizi wake na utekelezaji wake na gharama kubwa za uwekaji hereni za kielektroniki na inaona kuna haja ya kufanya upya tathmini ya zoezi hilo.’’

Aidha ameongeza kuwa, zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki lilipaswa kukamilika Oktoba 31, 2022 lakini hadi kufikia tarehe hiyo idadi ya mifugo iliyotambuliwa na kusajiliwa ilikuwa ni 5,068,617 ambayo ni sawa na asilimia 11, ya lengo la kutambua mifugo 45,920,000.’

Ng’ombe mwenye hereni za utambuzi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa, Serikali haijasitisha malipo kwa ajili ya huduma hiyo bali wamesitisha zoezi linalolalamikiwa, ili kupata nafasi ya kufanya tathmini ya mapungufu ya kikanuni yaliyowekwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo vizuri, kwa kushirikisha wadau wa mifugo.

Ameongeza kuwa, tayari Serikali imefungua soko la nyama katika nchi mbalimbali, kuondoa tozo kero na kuweka ruzuku kwenye dawa za kuogeshea mifugo na ujenzi wa mabwawa na malambo na akaongeza kwamba, ’’Natoa wito kwa wafugaji wote nchini kufuga kisasa ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nyama na mazao mengine kwa ajili ya masoko na uchakataji wa ndani na nje ya nchi.”

Polisi yachunguza tukio kupatikana kwa miili 21 ya wachimba migodi
Mawaziri G7 wakutana kuijadili Ukraine