Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul amesema Serikali inafanya utafiti ili kuona endapo kuna ulazima wa kufanya maboresho au marekebisho ya Sheria ya makosa ya kujamiana.
Gekul ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Thea Ntara aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itawasilisha Muswada wa Sheria ya adhabu kali kwa watu wanaobaka au kulawiti watoto na wanawake.
Amesema, kwa mujibu wa vifungu 130, 131, 131A na 154 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, ni makosa ya jinai kwa mtu kubaka na kulawiti na kwamba akosa yote haya adhabu yake ya juu ni kifungo cha maisha jela, na adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.
“Makosa yote haya yakitendeka dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela, pamoja na adhabu hizo Mahakama ina mamlaka ya kutoa amri ya ziada ya kumlipa fidia muathirika chini ya kifungu cha 131(1) cha Kanuni za adhabu,” amesema Gekul.