Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema hadi kufikia Juni 30, 2022 thamani ya uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa imefikia Sh.Trilioni 14.04.

Katambi ameyasema hayo hii leo Mei 16, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Halima Mdee aliyekata kujua tangu kuanzishwa kwa Mifuko hiyo ni kiasi gani cha fedha kimewekezwa na nini faida na hasara za uwekezaji huo.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema kiwango hicho ni kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa umewekeza Sh.Trilioni 6.03, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Sh.Trilioni 7.49 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Sh.Bilioni 521.94.

Ametaja faida za uwekezaji huo kuwa ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha Mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao na kusema, “uwekezaji huu huchangia pia kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi.”

Hata hivyo, Katambi amesema kama ilivyo katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi amabavyo vinaweza kusababisha hasara kwa baadhi ya uwekezaji, ambapo mifuko imevifanyia kazi kwa mujibu wa miongozo ya uwekezaji katika mifuko inayotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BOT).

Young Africans kuandika historia Afrika
Misaada yawasili Sudan vita ikizidi kushika kasi