Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans leo Jumatano (Mei 17) wanashuka dimbani kuikabili Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, katika Uwanja wa Royal Bafokeng.

Mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam juma lililopita, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa kipindi cha pili na Stephane Aziz Ki na Bernard Morison.

Young Africans inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote kuingia hatua fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo kwenye michuano ngazi ya Afrika.

Ingawa wapinzani wao Marumo Gallants wana rekodi nzuri kwenye uwanja wake wa nyumbani kwani hawajawahi kufungwa au kutoka sare katika michuano ya kimataifa msimu huu.

Katika dimba la Royal Bafokeng kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Marumo Gallants wameshinda bao 1-0 dhidi ya Pyramids ya Misri, mabao 3-2 dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya DRC, 4-1 dhidi ya Al Akhdar ya Libya na kisha kuwafunga USM Alger ya Algeria mabao 2-0.

Huku Young Africans wakiwa na rekodi nzuri katika michezo ya ugenini kwenye michuano hiyo kwani ukiondoa kufungwa mabao 2-0 na Monastri jijini Tunis na sare ya bao 1-1 na Real Bamako ya Mali, Young Africans wameshinda mechi zao zote za ugenini.

“Kila mchezaji afanye jukumu lake kwa kufuata maelekezo tunayowapa kuanzia mazoezini. Naamini tumefanya maandalizi mazuri na jukumu lao kwenda kuipa timu matokeo mazuri,” amesema Kocha Nasriddine Nabi akizungumzia mchezo huo.

Kwa upande wa Meneja Mkuu wa timu ya Marumo Gallants, Rufus Matsena amesema waliwapa Young Africans mabao mawili kwa ajili ya heshima ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere hivyo Young Africans watalazimika kuachia mabao matatu (3-0) kwa ajili ya kumuenzi Hayati Nelson Mandela.

China kuisadia Zanzibar sekta ya afya, miundombinu
Thamani uwekezaji mifuko hifadhi ni Trilioni 1.4 - Katambi