Serikali, inatarajia kuanza kupokea kero na maoni kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya wilaya 38 nchini, kuhusu utekelezaji na changamoto za upatikanaji wa umeme ili iweze kuzitafutia ufumbuzi na kuzitatua.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, January Makamba wakati akiongea na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam hii leo Julai 10, 2022 na kuongeza kuwa kero hizo ataanza kuzipokea kuanzia kesho Julai 11, 2022 wakati atakapoanza ziara yake ya siku 21 katika mikoa 14.
“Lengo la ziara mbali na maoni ni kukagua na kusimamia miradi inayotekelezwa na Wizara na mikoa mingine itahusika katika awamu ijayo ila katika maeneo haya nitazungumza na wananchi na kupokea kero na maoni ili kuimarisha utendaji wa sekta ya nishati,” amebainisha Makamba.
Amesema, kipaumbele katika ziara hiyo itakuwa ni kuelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, usambaaji wa umeme vijijini na Vitongoji pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo tajwa.
Ameyataja maeneo mengine ya kipaumbele katika ziara hiyo, kuwa ni uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi zake na usambazaji wa mafuta salama ya bei nafuu kwa wananchi ili kuzuia matumizi ya mafuta machafu.
Hata hivyo, Waziri Makamba amesema ziara hiyo itasogeza huduma za Wizara kwa wananchi hasa wale wa maeneo ya vijijini, ikiwemo kuongeza uelewa kwa Watanzania kuhusu sekta ya nishati na mageuzi yanayofanywa na Serikali.
Mikoa inayotarajiwa kunufaika na ziara hiyo kwa awamu ya kwanza, ni pamoja na Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, na Mtwara.