Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa miezi sita kwa wakazi wa maeneo ya Wilaya ya Kaliua iliyopo Mkoani Tabora kuhakikisha wanavuta nishati ya umeme wa REA majumbani mwao la sivyo atawachulia hatua baada ya msako atakaoufanya ukipita muda elekezi.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo hivi karibuni katika ziara yake ya kukagua mradi wa umeme wa REA wilayani Kaliua mkoani humo na kusema amesikitishwa na wananchi ambao hawataki kutumia umeme licha ya kuwa nguzo zimepita karibu na nyumba zao.
“Tunakoelekea sasa tutatumia nguvu haiwezekani serikali inatumia gharama kubwa kufanikisha mradi huu halafu mtu anashindwa kutumia umeme sasa leo ni mwezi wa kumi na mbili ikifika juni mwakani 2020 nitarudi tena hapa kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ambaye hajavuta umeme atavuta tu,” amefafanua Dkt. Kalemani.
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya umeme na hivyo kila mwananchi anapaswa kuonesha nia ya kupata nishati hiyo ili kuitimia katika shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato ikiwepo kufungua viwanda vidogo vidogo.
Aidha Dkt. Kalemani amesema wale wote ambao msako huo utawakumba atahakikisha anauza sehemu ya mali anazomiliki ili kupata pesa ya kuvuta umeme kwakua si vyema kukaa giza wakati nguzo zilizogharamiwa na serikali zinapita nje ya maeneo wanayoishi.
“Yaani tutauza chochote alichonacho ili kupata pesa ya kulipia tozo za ukamilishaji wa kuwekewa umeme awe na mbwa tutauza hata kambwa kadogo kadogo maana bei ya umeme ni rahisi mno,” amesisitiza Waziri Dkt. Kalemani.
Aidha katika hatua nyingine Dkt. Kalemani amewapongeza wakandarasi wanaosimamia mradi wa usambazaji wa umeme kakita eneo hilo kwa wakati na maeneo mengi na kusisitiza kuwa ifikapo Desemba 31 mwaka huu kila kijiji kiwe kimepata nishati hiyo.
Awali akiongea katika eneo hilo Mkandarasi wa zoezi hilo Joseph Fumbuka amemuhakikishia Waziri Kalemani kuwa watakamilisha kwa wakati usambazaji wa umeme katika vijiji vilivyosalia lengo likiwa ni kuhakikisha vinafikiwa na huduma hiyo.