Mamlaka za Serikali za Mitaa na watanzania kwa ujumla wametakiwa kutambua fursa, changamoto na mafanikio ya wanawake wanaoishi Vijijini ili kuweza kuwajengea mazingira mazuri ya kupata haki zao za msingi na kuwawezesha kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dokta John Jingu katika hotuba iliyowasilishwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia, Mboni Mgaza alipozungumza na waandishi wa Habari Mjini Morogoro kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke anayeishi Kijijini.

Hotuba hiyo imebainisha kuwa asilimia 65 ya wanawake wapo katika sekta ya kilimo janbo ambalo linaonesha kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji mazao ya kilimo na kuwa hali hii itasaidia kupiga hatua katika nchi, hivyo serikali kuweka miradi endelevu ya kuwaendeleza wanawake wanaoishi vijijini.

Aidha ameitaja Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu kuwa ni “Mwanamke anayeishi kijijini ni msingi na ustawi wa maendeleo ya nchi” ikilenga kumjengea uwezo mwanamke anayeishi kijijini kutambuliwa mchango wake katika ujenzi wa maendeleo kwa Taifa.

Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke anayeishi Kijijini huadhimishwa kila tarehe 15 Oktoba na mwaka huu, yatafanyika katika kijiji cha Kazole, kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, lakini kila Mkoa na Halmashuri zote nchini zitaadhimisha siku hii kwenye maeneo husika.

Prince Dube kulekea mchezo wa kesho dhidi ya Mwadui
Serikali kuzindua mpango wa kuendeleza viwanda