Serikali imedhamiria kupunguza gharama za kusafisha figo kutoka Shilingi 350,000 mpaka Shilingi 90,000 hadi 150,000 kwa lengo la kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za matibabu hasa kwa wenye vipato vya chini.   

Taarifa hizo zimetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kupitia Vijana, Mhe. Lucy Sabu lililohoji kuhusu mpango wa Serikali kupunguza gharama za kusafisha figo. 

Amesema, Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu ikiwemo huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa wote bila kujali kipato cha mgonjwa husika ambapo huduma hizo kwa sasa zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Hospitali Maalum ikiwemo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma. 

“Katika eneo la huduma za kusafisha figo, wizara imegundua kuna uwezekano wa kupunguza gharama za huduma hiyo badala ya kuwa 350,000 kwa awamu moja, mgonjwa ataweza kutibiwa kwa gharama ya kuanzia 90,000 hadi 150,000 kwa awamu moja, hivyo kuna mpango wa kushusha gharama hizo, amesema Naibu Waziri huyo.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye kipato kidogo kufuata taratibu zinazopelekea wao kupata misamaha ya huduma (exemption) ikiwemo huduma hii ya usafishaji wa figo kwa kuwasilisha barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata husika. 

Vile vile, Naibu Waziri Mollel amejibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania – NGOs, Neema Lugangira lililohoji kuwa Serikali imefikia wapi katika kufanya tafiti kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kubaini sababu zinazopelekea kuwa na wagonjwa wengi wa Kansa za aina mbalimbali ambapo alifafanua kuwa, zaidi ya Sampuli 700 za wananchi wanaoishi Kanda ya Ziwa zimekusanywa kwa ajili ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo cha kukithiri kwa ugonjwa wa Kansa katika maeneo hayo.

“Baada ya kukusanya sampuli hizo na kuzipeleka maabara, hatua tuliyoifikia kwa sasa ni kuzichambua sampuli hizo kwenye kiwango cha vinasaba ili tuweze kuona tatizo au sababu ya maeneo hayo kuathirika zaidi na ugonjwa huo,” amesema Dkt. Mollel.

Kocha Robertinho awataja Banda, Kibu, Sakho
Ibrahim Mutaz kuamua Nusu Fainali CAF CC