Mgomo wa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo umeibua mvutani bungeni kati ya wabunge na Serikali huku Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akiomba kupewa muda zaidi wa kujiridhidha kwa kile kinachoendelea katika soko hilo.

Hata hivyo majibu ya Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Dkt Ashantu Kijaji, kuhusu sakata hilo hayakuwaridhisha wabunge baada ya kujibu hoja ya Mbunge wa Makete Festo Sanga ya mgomo katika soko hilo ambapoa alijibu kuwa “Waliogoma Kariakoo ni kwa hiyari yao.”

Sanga, aliomba kutoa hoja ya kutaka Bunge lisitishe shughuli zake kwa muda ili lijadili kile alichosema kwamba “Kariakoo hali si nzuri” na kwamba Serikali inapoteza mapato kutokana na wafanyabiashara kufunga biashara zao.

Mbunge wa Makete Festo Sanga

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wafanyabiashara wa soko hilo wamegoma kutokana na mgogoro wa matumizi ya mashine ya kielekroniki (EFD), Kamatakamata na alichosema masuala ya usajili.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga (Chadema) aliunga mojo hoja hiyo ambapo alipinga majibu ya Waziri Dkt. Kijaji na kusema kuwa shughuli zimesimama hadi Alhamisi na wafanyabiashara watakaofungua biashara zao wametahadharishwa kuwa watajuta na kitakachowakuta.

Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda Dkt Ashantu Kijaji

Hata hivyo Dk Kijaji aliendeleza msimamo wake kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na timu ya watu kutoka Wizara ya Fedha wanaendelea na mazungumzo kwa ajili ya jambo hilo.

Kutokana na mvutano huo, Spika Tulia ameomba muda wa kufuatilia jambo hilo na kwamba akijiridhisha ataruhusu lijadiliwe bungeni wakati wowote.

Hata hivyo Spika amesema kwa kauli ya Waziri na hoja za wabunge ni wazi kuwa ndani ya Kariakoo kuna tatizo ambalo lazima lifanyiwe kazi ili kupata ufumbuzi.

Chelsea, Pochettino mambo safi, kazi kuanza 2023/24
Kapombe: Ninabaki Simba SC, nina deni kubwa