Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Zedliner Global Green Economy Partnership (ZGGEP) la nchini Marekani, Donovan Griay linalojishughulisha na uwekezaji wa Biashara ya Kaboni duniani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Mei 11, 2023 katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba jijini Dodoma, Dkt. Jafo amewahakikishia wawekezaji hao utayari na ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya kuanzisha miradi ya uwekezaji wa Biashara ya Kaboni nchini.
Dkt. Jafo amemueleza Rais wa ZGGEP kuwa, biashara ya kaboni kama nyenzo muhimu katika kukuza uchumi na kuibua fursa za maendeleo kwa wananchi ambapo kutokana na umuhimu huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Taasisi nyingine za Umma imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo.
Amesema Malengo makuu ya Kanuni na Mwongozo hiyo ni pamoja na kuweka utaratibu na masharti ambayo wadau na wajasiriamali wa biashara ya kaboni watapaswa kuzingatia wakati wa utekelezaji wa miradi mipya na miradi inayoendelea ya biashara ya kaboni katika sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kanuni na mwongozo huu unalenga kuweka mazingira rafiki ya usimamizi wa mazingira na biashara yaKaboni. Tunawakaribisha wawekezaji na milango yetu ya ushirikiano ipo wazi, tuna maeneo makubwa ya misitu, na maeneo mengine ya uoto wa asili yanayofaa kwa ajili ya biashara ya kaboni” amesema Dkt. Jafo katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wataalamu wa Ofisi ya Makamu wa Rais na wawekezaji wazawa kutoka Kampuni za Global International na GIS.