Serikali Mkoani Kagera imetenga zaidi ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya Vijana waendesha pikipiki maarufu kama (BODABODA) ili waweze kujiendeleza katika shughuli za ujasiliamali, na kuacha kutegemea shughuli moja.
 
Hayo yamesemwa mkoa Kagera na mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Marco Erisha Gaguti alipokuwa akizungumza waendesha pikipiki, wakati wa uzinduzi wa mashindano ya mpira wa miguu yajulikanayo kama JPM BODABODA CUP 2019, ambapo amewataka vijana hao kutumia fursa hiyo muhimu ili kuweza kujiinua kiuchumi.
 
“Vijana wana dhima na jukumu kubwa la kulinda amani ya nchi yetu kupitia shughuli wanazozifanya kikubwa ikiwa ni matumizi bora ya Vyombo vya Moto, Vijana wataelimishwa zaidi masuala ya Usalama barabarani, namna ya kujiepusha na uhalifu pamoja na elimu ya ujasiliamali,”amesema Gaguti
 
Aidha, ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo serikali inaimani kubwa kwamba upo uwezekano wa kupungua kwa majanga ya uhalifu kwasababu vijana hao watakuwa wamepewa elimu ya kuweza kuwatambua wahalifu na kusaidia kutoa taarifa na ushirikiano kwa jeshi la polisi pamoja na kupunguza ajali za barabarani.
 
Kwa upande wake mwenyekiti wa usalama barabarani mkoa wa Kagera, Euston Kabantega amewataka vijana hao kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wenzao waendesha bodaboda kwa kuhakikisha wanafuata na kutii sheria zote za usalama barabarani ili kuhakikisha wanakuwa salama wao pamoja na abiria wao wakati wa safari.
 
  • Hongereni kwa kufikia hatua hii ya Ujenzi- Majaliwa
 
  • Vijana watakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao
 
  • Video: Polisi wala sahani moja na ACT Dar, Mahakama ya Mafisadi yaanza kazi kwa kishindo
 
Mashindano ya JPM BODABODA CUP 2019 Kagera, yanayoratibiwa na Ofisi ya Mkuu Wa Mkoa Kagera kwa Kushirikiana na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani yataanza kutimua vumbi rasmi Jumamosi ya Tarehe 30, Machi mwaka huu kwa kuzishirikisha Timu 16 za Waendesha Bodaboda Manispaa ya Bukoba, huku zawadi zikitajwa kuwa ni pamoja na Kombe kwa Washindi Tatu Bora, pamoja na pesa Sh. Milioni 6 ambapo mshindi wa kwanza atajipatia kitita cha shilingi millioni 3, mshindi wa pili shilingi millioni 2 na mshindi wa tatu shilingi millioni 1

Video: Spika Ndugai alitekeleza sheria- Wakili Manyama
Lissu aielezea barua yake ya kudai mshahara wa kibunge