Waziri Mkuu wa Burkina Faso, Paul Kaba Thieba pamoja na baraza lote la mawaziri wamejiuzulu leo wakiacha nchi hiyo ikiwa na Rais pekee kwenye mhimili wa Serikali.
Rais wa nchi hiyo, Roch Marc Christian Kabore ametangaza hatua hiyo kupitia kituo cha runinga cha taifa lakini hakutoa sababu ya kufikiwa kwa uamuzi huo.
Thieba ambaye ni mchumi, amekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo tangu Januari 2016, alipoteuliwa na Rais Kabore na kuidhinishwa na Bunge.
Serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na msukumo mkubwa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya kigaidi pamoja na watu kutekwa wakiwemo viongozi mbalimbali.
Hivi karibuni, kufuatia kupotea kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa mashirika ya kimataifa, wanaharakati nchini humo walianza kumtaka Thieba na waziri wa ulinzi na usalama kuachia ngazi.
Edith Blais, mwanamke mwenye umri wa miaka 34 ambaye ni raia wa Canada pamoja na Luca Tacchetto mwenye umri wa miaka 30 ambaye ni raia wa Italia walipotea tangu Desemba mwaka jana.
Akitoa taarifa ya kujiuzulu kwa baraza hilo la mawaziri, Rais Kabore alieleza kuwa anawashukuru kwa kazi waliyoifanya na ushirikiano wao.
Alisema anategemea kuunda Baraza jipya mapema iwezekanavyo.