Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamaganda Kabudi, amesema vuguvugu linaloendelea nchini Afrika ya Kusini, hatuwezi kulielewa bila kuelewa historia ya nchi hiyo kwa sababu ni kwa kipindi kirefu wananchi wake walinyimwa haki zao chini ya ubaguzi wa rangi.
Waziri Kabudi ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika hafla maalumu ya kuwaaga vijana 100, wanaokwenda nchini Israel kwa ajili ya mafunzo ya kilimo kwa vitendo na kusema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunga mkono kauli ya kulaani vitendo hivyo iliyotolewa na Rais wa nchi hiyo Cyrill Ramaphosa.
”Serikali ya Tanzania inaunga mkono kauli iliyotolewa na Rais wa Afrika ya Kusini Cyrill Ramaphosa ya kulaani vikali na kukemea vitendo hivyo na serikali inaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na Serikali ya Afrika Kusini kwani vuguvugu hizo zimetia doa nchi hiyo,” amesema Profesa Kabudi.
Hadi sasa vimeripotiwa vifo vya watu takribani watano, huku wengine wakijeruhiwa pamoja na kuharibiwa mali zao, vurugu ambazo zinafanywa na baadhi ya vijana wazawa kwa madai ya kwamba Waafrika kutoka nchi zingine wanawachukulia ajira na kazi zao.