Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Faustine Ndugulile amesema kuwa Wizara yake iko mbioni kupeleka Bungeni muswada utakaowezesha kutungwa kwa Sheria ya kulinda taarifa binafsi ili kulinda faragha na taarifa za mwananchi.
Dkt. Ndugulile ameyasema have bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu mijadala mbalimbali iliyotolewa na Wabunge kwenye semina iliyotolewa kwao kuhusu huduma za mawasiliano na intaneti ili waweze kufahamu namna Wizara inavyotekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake.
Ameongeza kuwa Wizara inaandaa sheria hiyo ili kulinda faragha na taarifa binafsi za wananchi katika hatua ya ukusanyaji wa taarifa, usafirishaji, matumizi na utunzaji wa taarifa hizo kwa kuwa taasisi mbalimbali zinatumia taarifa husika hivyo amewataka Wabunge kuwa tayari pindi pendekezo la muswada litakapowasilishwa Bungeni ili sheria hiyo iweze kutungwa kwa maslahi mapana ya taifa.
“Hivi sasa ujambazi umehama kutoka silaha za mkononi na kuhamia mtandaoni, Serikali itaendelea kuelimisha wananchi, kuboresha mifumo na teknolojia ili nchi iwe mbele zaidi katika kudhibiti uhalifu mtandaoni,” amesema Ndugulile.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Kakoso ameishauri Serikali iongezee fedha za kuuwezesha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa ruzuku ya kutosha kwa kampuni za simu ili mawasiliano yafike kwa wananchi wote ikiwemo kuongeza usikivu wa redio kwenye maeneo ya mipakani.