Serikali imetaka kupuuzwa kwa taarifa zinazosambazwa mitandaoni na katika chombo cha habari kutoka nchi jirani ya Kenya zinazosema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameachia wafungwa wa kisiasa.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kuingilia mahakama na kwamba Tanzania haina wafungwa wa kisiasa.
Taarifa hiyo pia iliripoti kuwa Rais amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwaachia Wafungwa hao ambao Msemaji amesema Rais hawezi kuingilia mchakato wowote wa Mahakama.
“Kuna jambo tumeona tulitolee ufafanuzi, kuna clip inazunguka ikisema Rais Samia Suluhu ametoa agizo la kuachiwa huru kwa Wafungwa wa Kisiasa 23, sio kweli Rais hajazungumza suala hilo, pili nchi yetu haina Wafungwa wa Kisiasa, Watanzania wapuuze taarifa hizo,” amesema Msigwa.
“Hiki Chombo cha Habari cha Nchi jirani nisingependa kukitaja tunaamini wataomba radhi na kufuta taarifa hiyo, tayari Ofisi yetu ya Ubalozi Nairobi inafuatilia kujua kwanini wamepotosha,” ameongeza Msigwa.
Msigwa amesema kuwa hatua mbalimbali za kisheria zinafuatwa, kufuatia usambazwaji wa taarifa hizo za uongo.