Serikali imezitaka mamlaka kupitia halmashauri zote nchini kuhakikisha watu binafsi, makampuni na viwanda kutohujumu miundombinu ya umma ili kufanikisha biashara ya chuma chakavu.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma hii leo Desemba 23, 2019 na Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira, George Simbachawene wakati akitoa taarifa za kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2019, udhibiti na usimamizi wa taka za kielektroniki na ada na tozo za usimamizi wa mazingira za mwaka 2019.

Amesema hatua iliyochukuliwa ya kufanya marekebisho katika kanuni hizo ikiwemo kuweka mfumo bora wa kisheria utakaosimamia taka hatarishi mbali na lengo la kuhakikisha mazingira yanalindwa na kusimamiwa kikanuni pia inakusudia kulinda miundombinu ya nchi kiufasaha.

“Baadhi ya watu au makampuni vikiwemo viwanda, waaache kuhujumu miundombinu ya umma ili kufanikisha biashara yao ya chuma chakavu na katika hili mamlaka husika zinatakiwa kusimamia sheria na kanuni za udhibiti wa taka hatarishi ili kuondoa uchafuzi wa mazingira,” amefafanua Waziri Simbachawene.

Amesema taka hatarishi ni pamoja na chuma chakavu na kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara na watu ambao sio waaminifu wanaofanya biashara hiyo bila kuwa na vibali husika huku walio na vibali baadhi yao wakiwa hawafuati masharti yaliyowekwa kisheria.

Aidha Simbachawene amewataka baadhi ya wafanyabiashara walio na tabia ya kukwepa ulipaji wa kodi stahiki kuacha vitendo hivyo mara moja kutokana na serikali kuweka mfumo wa kiutawala, kisheria na kikanuni ambao sio rahisi kufanya udanganyifu bila kugundulika.

“Na katika kuboresha usimamizi wa mazingira tumefanya marekebisho ya kanuni mbalimbali pamoja na kutunga kanuni mpya zikiwemo zile za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2009 na sheria hizi zitasimamiwa ipasavyo,” ameongeza Simbachawene.

Amezitaja kanuni nyingine kuwa ni tozo za usimamizi wa mazingira za mwaka 2008, marekebisho yake ya mwaka 2016 na 2018 sambamba na kuandaa kanuni mpya za udhibiti na usimamizi wa taka za kielektroniki za mwaka 2019.

Hata hivyo Simbachawene amebainisha kuwa kanuni mpya za mwaka 2019 zimeainisha aina ya shughuli za usimamizi wa taka hatarishi ambazo zinapaswa kuwa na kibali cha waziri mwenye dhamana ya mazingira huku akitaja shughuli zinazopaswa kuombewa kibali ndani ya nchi kuwa ni kukusanya, kutunza, kusafirisha na kumiliki au kuendesha mtambo wa usimamizi wa taka hatarishi.

Aidha ameongeza kuwa kanuni hizo zimeweka adhabu kwa makosa ya kutokuwa na kibali cha kusimamia taka hatarishi nchini zikiwemo faini kuanzia shilingi milioni tano hadi bilioni 10 au kifungo kisichozidi miaka 12 au vyote kwa pamoja.

Viwanja 208 vya ndege nchini vyapigwa 'stop'
Magufuli aagiza vijana 800 wa JKT kuajiriwa