Serikali nchini, imeumaliza mgogoro wa matumizi ya ardhi Wilayani Mbarali mkoani Mbeya uliodumu kwa miaka 15, ambao ulihusisha wakazi wa Wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akizungumza na wadau, wawekezaji wa Bonde la Usangu, wakulima wa mpunga, wamiliki wa mashine za kukoboa mpunga na wafugaji Januari 16, 2023 Mkoani Mbeya, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wamefanya maboresho ambayo yatawawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu.
Amesema, marekebisho ya tangazo hilo pia yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka ikiwemo kutoa eneo la hekta 74,000 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
“Hii GN 28 Serikali tumeamua kuitafutia ufumbuzi baada ya vikao vingi na wadau kwa faraja kabisa nataka niwaambie tumefikia hatua nzuri itakayowezesha kila anayejishughulisha na kilimo kuendelea na kilimo chake na kila anayejishughulisha na mifugo kuendelea na ufugaji yake,” amefafanua Waziri Mkuu.