Baada ya kumaliza Kambi ya majuma mawili Dubai-Falme za Kiarabu, Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ameonesha kuwa na matuamini makubwa ya kuwa na kikosi tishio kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC imefuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, ikipangwa Kundi C sambamba na Mabingwa wa Uganda Vipers SC, Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).

Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema wachezaji wake wameonesha ukomavu kupitia Programu ya Mazoezi aliyoitumia wakati wa kambi yao huko Dubai, huku wakicheza michezo miwili ya Kimataifa ya Kirafiki dhidi ya Dhafra FC na CSKA Moscow.

Amesema kuna mambo mengi ya kiufundi yameongezeka kwenye kikosi cha Simba SC, ambayo anaamini yanakwenda kuleta chachu mpya ya ushindani kwenye klabu hiyo ya Msimbazi.

“Hii timu sasa inakwenda kufanya makubwa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, achana na kuwa ina rekodi na historia nzuri kwenye michuano hiyo, ila kuna kitu kimeongezeka kwa siku tulizokuwa Dubai.”

“Unaweza ukaona kwenye mchezo wetu dhidi ya CSKA Moscow, ile ni timu bora duniani lakini tumeweza kupata sare, kipindi cha pili wachezaji walicheza kwa nguvu na kufuata maelekezo ambayo niliyatoa kwao. Hiyo ndiyo timu inatakiwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.” amesema Robertinho

Tayari Simba SC imeshaanza safari ya kurejea jijini Dar es salaam ikitokea Dubai-Falme za Kiarabu, na kesho Jumatano (Januari 18), itacheza mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku nne
Serikali yamaliza mgogoro wa Ardhi Bonde la Usangu