Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imekamilisha malipo ya ununuzi wa ndege mpya tatu.
Majaliwa amesema hayo wakati akitoa hoja bungeni juu ya makadirio na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Majaliwa amesema kuwa ndege hizo zinatarajiwa kuwasili katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 na hivyo kuwezesha serikali kuwa na ndege zake 12.
“Serikali imekamilisha malipo ya ununuzi wa ndege tatu. Ndege hizo zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/22 hivyo kufanya serikali kuwa na ndege 12,”- amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amelipongeza shirika la Ndege la ATCL kwa kuanzisha safari za kwenda nje ya nchi Guangzhou China, akisema kuwa safari hizo ni chachu ya kuimarisha biashara, utalii na ajira.