Serikali nchini, imeahidi kuboresha zaidi sekta ya mifugo kupitia njia mbalimbali huku ikiwa na nia ya kuona vijana wanafanya uzalishaji wa mali kwa kuingia katika sekta ya mifugo.

Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega amebainisha hayo katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madume ya ng’ombe 36 aina ya boran Heifer kwa Halmashauri ya Buchosa.

Amesema lengo la serikali ni kuona vijana wanafanya uzalishaji wa mali kwa kuingia katika sekta ya mifugo na kupeleka mifugo hiyo sokoni.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (Mb), akikagua na kusikiliza maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa mabanda yatakayotumika kufugia ng’ombe kwa wanafunzi wa Kituo Atamizi cha Mabuki kilichopo Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza kupitia program ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI).

‘’Nchi yetu ina ng’ombe milioni 33 na bado tija ipo chini sana kutokana na viwanda vingi havipati malighafi ya kutosha. Mifugo inatakiwa kuongeza tija na pato la taifa na kwa mtu mmoja mmoja,’’ Amesema Ulega.

Aidha, ameongeza kuwa kupitia programu maalum ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI), Serikali imefanikisha kuanzisha mafunzo ya unenepeshaji mifugo ambapo takriban vijana 70 wanapatiwa mafunzo hayo kwa vitendo katika Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Wilayani Misungwi.

Unenepeshaji mifugo kwa vitendo kwenye vituo atamizi wakati alipofika katika Kituo cha Mabuki kilichopo Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Waziri Ulega amesema, serikali imeanzisha vituo atamizi vya SAUTI ambapo mpaka sasa kuna vituo nane kwa ajili ya vijana kufunzwa na kwamba kupitia vituo hivyo atamizi vijana watafundishwa namna bora na kisasa ya kutengeneza mashamba ya malisho na upatikanaji wa mifugo bora.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga aliishukuru serikali kwa kuipatia Halamshauri hiyo ya Buchosa Ng’ombe, huku mmoja wa wanafunzi hao akiishukuru serikali kwa kuja na programu hiyo ya ufugaji ambayo itawasaidia kupata ajira.

Makamu wa Rais akaribisha uwekezaji sekta ya Utalii, Kilimo
Serikali yasisitiza uzingatiaji sheria usimamizi wa mazingira