Serikali nchini, imeshauriwa kuangalia upya kanuni na sheria za uhifadhi wa Mazingira na kuzibadilisha ili ziendane na uhalisia wa matokeo ambaye ya sasa ambayo yameathiri maeneo mengi yaliyokosa mvua za kutosha na kuwa makame kutokana na uharibifu uliofanywa na binadamu.
Ushauri huo umetolewa hii leo Desemba 19, 2022 na mdau wa Mazingira na Mkongwe wa Sanaa ya uimbaji nchini, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 kwenye Kongamano la Wahariri na Wadau wa uhifadhi, Mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Amesema, “Mtu anakamatwa anachepusha maji, mwingine anachunga ng’ombe mwingine analima pembeni kwenye vyanzo vya maji, hawa wote wanakimbilia kulipa faini na kama adhabu zipo basi hazitoshi maana uharibifu ni mkubwa sana me naona sheria zetu ziangaliwe upya Serikali itafakari.”
Aidha, Afande Sele pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kusimamia na kupambana ili kuhahikisha nchi inakuwa salama na mapambano dhidi ya majangili wa uhifadhi wa mazingira yanakuwa yenye mafanikio.