Ili kudhibiti mfumuko wa bei, Serikali imesema baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa (Februari 9, 2023), hali ya mfumuko wa bei za bidhaa haitakua kama ilivyo sasa kutokana na uwekaji wa mikakati ya kudhibiti mfumuko wa bei na uzalishaji na kikodi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye amezitaja hatua hizo ambazo zilizochuliwa na Serikali huku akisema ruzuku iliyotolewa kwenye mbolea na mafuta na mazao yatakayozalishwa katika maeneo yaliyotumia ruzuku yatakuwa kwa bei nafuu kuliko yale yanayozalishwa bila bei ya ruzuku.
Amesema, “Haya mazao tunayotumia sasa hivi ni yale yaliyozalishwa mwaka jana, yaliyozalishwa kwa mbolea isiyokuwa na ruzuku, maana yake walitumia Sh120,000 hadi Sh140,000, mafuta hayakuwa na ruzuku, ndiyo yaliyokuwa juu na yalitumika katika usafirishaji na uzalishaji katika baadhi ya maeneo.”
Aidha, ameongeza kuwa, ukame uliokuwepo mwaka jana pia ulisababisha upungufu ambao kwa asili katika uchumi huwa ni chanzo cha mfumuko na kwamba upungufu huo pia tunatarajia utadhibitiwa kwa waliopata ruzuku, hivyo watazalisha zaidi kutokana na gharama kuwa chini.
Dk Mwigulu amebainisha kuwa,”sehemu zote zikipata mvua vizuri na mbolea kutumika vizuri tunatarajia suala la upungufu wa mavuno halitakuwepo, tutakuwa tumeongeza mavuno na kushusha gharama za uzalishaji kwa kutumia ruzuku zilizotolewa.”
Amesema hatua za muda mfupi zilizochukuliwa ni kutoa akiba ya mazao yaliyokuwepo huku akieleza suala hilo litaendelea ameeleza kuwa hivi sasa pia Serikali inawaza kuanza kununua mchele kuwa sehemu ya akiba ya Taifa ili na wenyewe uwe unatolewa kwa ajili ya kwenda kupunguza bei ya bidhaa hizo zinapokuwa sokoni.
“Tunaamini baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa, hali ya mfumuko wa bei za bidhaa haitakua kama ilivyo sasa na waliohifadhi mazao wakiamini bei zitazidi kupanda niwasihi wayatoe sasa maana kwa hatua ambazo tunaendelea kuzichukua inawezekana bei ikawa chini kuliko wanavyotarajia,” amesema Mwigulu.
Kulingana na Mwigulu, amebainisha kuwa Mawaziri wa fedha wa Afrika ya Mashariki wamejadili juu ya namna wanavyoweza kupunguza gharama za uingizaji ili kupata bidhaa zinazotoka maeneo mengine
“Kwetu sisi bidhaa hizo hazijaja lakini kwa sababu sisi tulikuwa tunalisha ukanda mwingine uamuzi huo unatupa ahueni kwa sababu sisi tulikuwa tunalisha ukanda mkubwa,” amesema Dk Mwigulu.