Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema majeruhi mmoja kati ya 26 wa ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea mjini Bukoba, bado yupo Hospitali na kwamba wengine wamepona na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Msigwa ameyasema hayo hii leo Novemba 8, 2022 Mkoani Kagera, na kuongeza kuwa katika ajali hiyo waliokolewa walikuwa ni watu 26, waliopelekwa Hospitali 24 na wawili hawakufika kupata matibabu kwa kuwa walipata majeraha madogo.
Amesema, “Kati ya hawa Majeruhi 24 waliolazwa Hospitali, mmoja tu ndio yupo Hospitali na wengine 23 wameruhusiwa, huyu aliye Hospitali afya yake inaendelea vizuri na ataruhusiwa kurudi nyumbani baada ya afya yake kuimarika.”
Wakati huo huo, Kijana Majaliwa Jackson aambaye aliwaokoa Watu 24 kwenye ajali hiyo tayari amepokelewa na Jeshi la Zimamoto na anatarajia kuanza mafunzo ya Zimamoto na Uokoaji pamoja na ya Uaskari katika Chuo kilichopo Chogo, Handeni Mkoani Tanga.