Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limempokea kijana Jackson Majaliwa aliyeokoa abiria 24 katika ajali ya ndenge ya Precisison Air iliyotokea Ziwa victoria Mkoani Bukoba Novemba 6, 2022, na anatarajiwa kuanza mafunzo katika chuo cha Chogo kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga.

Majaliwa, ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza dagaa katika mwalo wa Nyamkazi uliopo katika manispaa ya Bukoba, alionyesha ujasiri wa kwenda kwenye ndege hiyo iliyoanguka haraka na kufanikiwa kuvunja mlango wa ndege na kuokoa abiria 24.

Wakati wa kuaga miili ya watu 19 waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kijana huyo akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili aingizwe kwenye Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kupatiwa mafunzo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayaimisi, tayari kijana huyo amepokewa na jeshi hilo na atapewa mafunzo rasmi ya zimamoto, uokoaji na uaskari.

“Mkuu wa Jeshi wa Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Jenerali John Masunga anaujulisha umma kuwa Majaliwa Jackson Samweli, ameshapokelewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Hivyo, maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yameshatekelezwa.

“Majaliwa anatarajiwa kuanza mafunzo ya zimamoto na uokoaji pamoja nay a uaskari katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo, wilaya ya Handeni mkoani Tanga,”

“Kamishna Jenerali anatoa pole kwa wafiwa wote na kumwombea faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia, anawatakia majeruhi wote afya njema. Anawasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto katika kuokoa maisha ya watu na mali dhidi ya majanga mbalimbali,” amesema Nzalayaimisi.

Rwanda yadai DRC 'imeanza tena' uchokozi
Picha: Ndege iliyopata ajali yatolewa ziwani