Meya wa New York, Eric Adams ametangaza hali ya dharura mjini humo hutokana na kuenea kwa virusi vya Monkeypox.
Kupitia taarifa iliyotolewa ikiwa kama amri ya kiutendaji, Adams amesema hatua hiyo itaimarisha juhudi za kuhamasisha utoaji chanjo na matibabu kwa watu wengi ili kuhakikisha mlipuko huo unadhibitwa kwa wakati.
Amri hiyo, inampa Adams madaraka ya kusitisha baadhi ya sheria za mji na kuweka nyingine za muda, ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi.
Awali, gavana wa jimbo hilo Kathy Hochul, alitangaza hali ya dharura ya jimbo akisema katika wiki nne hadi sita zijazo, Serikali kuu itatoa chanjo 110,000 ili kuongeza kwenye 60,000 zilizopo.
Mpaka sasa, mji wa New York ulikuwa umeripoti kesi 1,472 za virusi vya Monkeypox kwa mujibu wa mtandao wa afya unaokusanya data mjini humo.