Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka nchi za nje pamoja na wadau wa maendeleo kuwekeza katika viwanda vya dawa nchini ikiwa ni hatua ya kuboresha upatikanaji wa dawa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi aliyaalika mashirika ya kimataifa, jana, Septemba 24, 2019 alipokuwa akizungumza katika mkutano wa viongozi wa ngazi ya juu kuhusu upatikanaji wa huduma za afya, katika Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika jijini New York nchini Marekani.
Prof. Kabudi alielezea hatua ambazo Tanzania imezichukua kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kuwa ni pamoja na kuanzisha mifuko miwili ya bima ya afya, ambayo ni mfuko wa Taifa wa bima ya afya na mfuko wa bima ya jamii. Alifafanua kuwa hadi sasa mifuko hiyo imeleta unafuu mkubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Aliongeza kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na serikali kuimarisha huduma za afya ni pamoja na kuongeza na kujenga vituo vya afya vipya zaidi ya 300, hospitali za wilaya zaidi ya 70 pamoja na ukarabati wa makazi ya wahudumu wa afya zaidi ya 301 ili kuhakikisha huduma za afya zinasogezwa karibu na wananchi na zinapatika kwa wakati wote.
Aidha Prof. Kabudi ameueleza mkutano huo kuwa Tanzania kwa sasa imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba,hatua ambayo mpaka hivi sasa kwa mwaka huu pekee takribani viwanda vinane vya dawa vinajengwa Tanzania ambavyo vitawawezesha watanzania wengi kupata dawa kwa bei nafuu.
Pia kumekuwa na ongezeko katika upatikanaji wa huduma za dawa muhimu (essential drugs) 321 ambazo upatikanaji wake umefikiwa asilimia 75% hadi mwaka 2019,ambapo Prof. Kabudi amesema kuwa jitihada hizo zimesaidia utoaji wa chanjo kwa watoto na kupunguza vifo vya malaria kwa watoto wachanga ambapo pia maradhi ya malaria na maambukizi ya ukimwi kwa kiasi kikubwa yamepungua.
Mkutano huo umetoa fursa kwa nchi wanachama kuelezea hatua iliyofikiwa katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.
Hatimaye, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walipitisha tamko la kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi yote katika jamii pamoja na mambo mengine, tamko hilo pia limeainisha vipengele kwa nchi wanachama kufuata kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya afya, upatikanaji wa dawa, kupungua kwa maambukizi, kutenga bajeti ya kutosha kwenye sekta ya afya na kuboresha mifumo ya kisera kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa watu wote.