Gundu limeendelea kumuandama meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer, kufuatia matokeo mabaya yanayokikumba kikosi chake, katika mshike mshike wa ligi kuu ya England.

Joto la kubaki ama kutimuliwa kwa meneja huyo kutoka nchini Norway, lilipanda mwishoni mwa juma lililopita, baada ya kupoteza mchezo dhidi ya West Ham United kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri, jijini London.

Hatua ya kupoteza mchezo huo, iliifanya klabu hiyo ya Old Trafford kuachwa kwa tofauti ya alama 10 na vinara Liverpool, kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuchezwa michezo sita tu.

Mashabiki wa Manchester United wanaamini umefika wakati wa Ole Gunnar Solskjaer, aliyekuwa shujaa wakati akiitumikia klabu hiyo kama mchezaji, kuondoka na nafasi yake kupewa meneja mwingine.

Rekodi za Ole kwenye michezo ya ligi inatia wasiwasi mkubwa. Akiwa meneja wa kikosi hicho, michezo 45 aliocheza kwenye ligi, ameshinda 17, sare tisa na kuchapwa mara 19. Hiyo ina maana Ole amepoteza michezo mingin kuliko alioshinda. Ameshinda pia mabao 61, lakini akifunga mabao 73.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya magazeti nchini England yameanza kutoa orodha ya mameneja ambao wanadhaniwa kuwa dawa kuiokoa Manchester United, endapo Ole Gunnar Solskjaer atatimuliwa.

Thomas Tuchel
Meneja mbunifu anaefanya mambo yake huko Paris Saint-Germain. Kitendo cha kuweza tu kuwamiliki wachezaji mastaa kama Neymar, Kylian Mbappe, Edinson Cavani na mastaa wengine kwenye kikosi chake huo ni ukomavu tofauti kabisa ambao unamfanya kuwa chaguo sahihi na kutua huko Old Trafford. Kunasa huduma ya Tuchel itakuwa kama Liverpool walipomchukua Jurgen Klopp, kuna kitu atakuja kukifanya Man United.

Mauricio Pochettino
Meneja wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino kupata dili la kwenda kuinoa Man United bila ya shaka hiyo itakuwa kazi ya ndoto zake. Kabla ya Ole kupewa kazi, Pochettino alipewa nafasi ya kwenda kuinoa timu hiyo, lakini sasa Muargentina huyo anatazamwa kama mtu wa kwenda kuokoa jahazi.

Massimiliano Allegri
Moja ya mameneja bora kabisa wasiokuwa na kazi kwa sasabaada ya kuachana na Juventus mwishoni mwa msimu uliopita, lakini kazi yake haina mjadala. Ni meneja aliyeonyesha anaweza kutokana na mafanikio aliyopata Juventus na AC Milan, huku akiwa na uzoefu na kucheza soka tamu ukilinganisha na Solskjaer. Ni chaguo sahihi kama atatua Old Trafford.

Laurent Blanc
Kwa muda mrefu, Mfaransa Blanc amekuwa hana kazi. Lakini, meneja huyo wakati wa enzi zake akiwa mchezaji, alicheza Man United, hivyo bila ya shaka anafahamu utamaduni wa timu hiyo. Blanc pia amekuwa na uzoefu wa kubeba mataji, baada ya kufanya hivyo akiwa PSG na Bordeaux alikonyakua ubingwa wa Ligue 1 kabla ya kupata ukomavu zaidi wa kuitoa timu ya taifa ya Ufaransa. Ana rekodi nzuri kuliko Ole.

Mameneja wengine
Orodha ya mameneja ambao wanadaiwa kwamba watakuwa na mambo tofauti watakapotua Old Trafford ni pamoja na Arsene Wenger, ambaye hana kazi kwa sasa, Erik ten Hag wa Ajax, Julian Nagelsmann wa RB Leipzig, Jesse Marsch wa RB Salzburg na Brendan Rodgers wa Leicester City.

Tetesi za soka: Zaha kuihama Crystal Palace mwakani
Serikali yawafungulia milango zaidi wawekezaji kwenye viwanda vya dawa