Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema ushirikiano wa pamoja baina yake, wananchi na wadau mbalimbali umefanikisha kuudhibiti ugonjwa wa Marburg ulioripotiwa kuzuka
Mkoani Kagera Machi 21, 2023.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hii leo Aprili 29, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huo Mkoani Kagera na kuongeza kuwa uwepo wa mafanikio hayo ni jambo la kumshukuru MUNGU.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Amesema, “nafurahi kuwajulisha kuwa kuanzia tarehe 21 Aprili 2023 hatuna mgonjwa yeyote mwenye virusi vya ugonjwa huu mkoani Kagera hapa nchini Wagonjwa wawili waliokuwa wamesalia katika vituo maalum vya matibabu waliruhusiwa kutoka Aprili 20 na 21, 2023 baada ya kuthibitika kimaabara kuwa hawana tena virusi vya Marburg.”
Aidha, ameongeza kuwa, “nilipotoa taarifa yangu ya mwisho kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu, tulipata ongezeko la mgonjwa mpya mmoja ambaye ni mama wa mtoto wa umri wa miezi 18 aliyekuwa ametengwa na baadaye kuthibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Marburg,” amesisitiza.