Serikali nchini, imesema inawafuatilia na itawachukulia hatua matapeli wanaosambaza taarifa za uongo kuhusu kuwarejesha katika Utumishi wa Umma watumishi waliobainika kughushi vyeti na kuondolewa katika Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama wakati akielezea uamuzi huo kufuatia taarifa za uongo zilizosambazwa na matapeli, kuwa Serikali imefanya uamuzi wa kuwarejesha watumishi walioondolewa kazini kwa kosa la kughushi vyeti.
Amesema, mara kadhaa ofisi yake imekuwa ikikanusha taarifa ya uongo inayotolewa na matapeli kwa masilahi yao binafsi, taarifa ambayo imekuwa ikibadilishwa tarehe mara kwa mara lakini maudhui ni yale yale.
Aidha, kufuatia usumbufu unaotokana na usambazaji wa taarifa za uongo, Waziri Jenista ametoa onyo kwa matapeli wanaoendelea kuupotosha umma kuacha mara moja na kuongeza kuwa watakaoendelea kukiuka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.