Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddin Mohamed Nabi huenda akamtumia Beki kutoka nchini Mali Mamadou Doumbia kwenye mchezo wa Hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Young Africans itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kuikaribisha Rhino Rangers ya Tabora, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara.

Doumbia tangu aliposajiliwa Young Africans kupitia Dirisha Dogo, hajawahi kuonekana kwenye mchezo wa Mashindano, huku sababu kadhaa zikitajwa na Uongozi wa Klabu hiyo kupitia Idara ya Habari na Mawasilino.

Mkuu wa Idara hiyo Ally Kamwe amesema, Beki huyo aliyetua klabuni hapo akitokea Stade Malien ya nchini kwao Mali, ameshakamilisha taratibu zote za kupata vibali vya kuanza kazi klabuni hapo, pia amefanya maandalizi ya kucheza mchezo dhidi ya Rhino Rangers kesho Jumapili (Januari 29).

“Kilichobaki ni kwao Benchi la Ufundi, lakini kwa upande wa Uongozi taratibu zote za vibali zimeshakamilishwa”

“Kwanza kabisa Benchi la Ufundi lilitaka kumuona kwenye mzoezi, siku aliyofika Dar es salaam ilikuwa ni usiku sana, kesho yake hakufanya mazoezi kwa sababu alikuwa amechoka na ilikuwa siku moja kabla ya mchezo na Ruvu Shooting, ndiyo maana hakucheza.”

“Pia hakufanya mazoezi na timu, hajajua muundo wa timu na ukiangalia safu yetu ya ulinzi hatukuwa na uhitaji huo wa haraka wa kumtumia.”

“Kwenye mchezo unaokujaa wa Kombe la FA dhidi ya Rhino Rangers, tunaweza kumuona akiwa anacheza.” amesema Ally Kamwe

Serikali yawatumia salaam matapeli mitandaoni
Hamis Juma Mbizo 'H-Mbizo' afariki Dunia