Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amewataka Wanachama wa klabu hiyo kuchagua viongozi sahihi ambao watafanikisha malengo ya Klabu.

Mkutano mkuu wa Uchaguzi Simba SC umepangwa kufanyika Kesho Jumapili (Januari 29) katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere ‘JNICC’ jijini Dar es salaam.

Try Again amesema Wanachama wa Simba SC wenye sifa wa kupiga kura kwa mujibu wa Katiba ya Klabu hiyo, wanapaswa kutumia haki yao kuchagua viongozi ambao watakuwa na maono ya kuifikisha mbali klabu hiyo.

Amesema jukumu la Wanachama ni kusikiliza sera na kufanya maamuzi ambayo yatakinufaisha kizazi cha sasa na cha baadae, ili kuiwezesha Simba SC kuwa klabu kubwa na yenye mafanikio ndani na nje ya Tanzania.

“Huu ni wakati mzuri kwa Wanachama wa Simba SC kutumia vizuri haki yao ya Uchaguzi kwa kupata viongozi imara na kuendeleza kauli mbiu yetu ya NGUVU MOJA ili kufanikisha malengo ya klabu.”

“Jukumu la Wanachama ni kuhakikisha wanaitendea haki Klabu ya Simba SC, tunatakiwa kuwa na viongozi ambao wataipeleka mbele klabu yetu, Klabu hii ina maono makubwa ya kuwa Klabu yenye mafanikio ndani na nje ya Tanzania.” amesema Try Again

Wanachama wa Simba SC watawachagua Mwenyekiti na Wajumbe ambao wote wataingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi kuungana na Wajumbe wengine wanaotokana na Mwekezaji wa klabu hiyo.

Mwenyekiti atakayechaguliwa atakuwa na nafasi kuchagua wajumbe wawili na kufanya kufikia nane kwa mujibu wa Katiba ya Klabu hiyo.

Wagombea nafasi ya Mwenyekiti wapo wawili ambao ni Advocate Moses Kuluwa na Murtaza Mangungu anayetetea nafasi yake.

Wajumbe ni Seif Muba, Seleman Haroub, Idd Katete, Issa Masoud, Abubakari Zebo, Abdallah Mgomba, Edward Mweladzi, Rashid Khamsini, Asha Baraka, Pendo Aidan na Aziz Mohamed.

Caicedo atuma waraka Brighton & Hove Albion
Serikali yawatumia salaam matapeli mitandaoni