Serikali imezidi kuwabana wakwepa kodi mara baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutengeneza mfumo mpya wa ukusanyaji maduhuli kupitia mashine za kielektroniki (EFDMS) ambao utasaidia kukusanya mapato yote na yale yasiyo ya lazima.
Hayo yamesemwa na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Neema Mrema wakati wa semina ya kodi kwa Idara na Taasisi za Serikali iliyofanyika Jijini Dar es salaam,
Amesema kuwa ili nchi iweze kufikia uchumi wa kati na wa viwanda ni lazima kila mhusika aweze kuwajibika katika kulipa kodi, kwakuwa mfumo huo mpya utasaidia kuweza kuinua pato la taifa kwa kiasi kikubwa.
Aidha, amesema kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuimarisha miamala na risiti zote zitakuwa na saini za kielektroniki na ‘QR Code’, hivyo kughushi risiti kutoka katika mashine ambazo hazijasajiliwa haitawezekana .
“EFDs zilitengenezwa kwa ajili ya kodi ya ongezeko la thamani, mashine za sasa zimeboreshwa ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato yeyote kutoka kwa wafanyabiashara na taasisi za Serikali,”amesema Mrema.
Hata hivyo, Mrema amesema kuwa utaratibu wa mfumo huo mpya utaweza kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi katika taasisi na mashirika mbalimbali. taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali.