Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amelaani mauaji ya Askari Polisi 8 waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.

“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu 8 ambao  wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.” amesema Rais Magufuli

Tukio hilo limetokea jana wakati Askari Polisi hao walipokuwa wakitoka kubadilishana doria ambapo wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi.

“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.

Pia, Rais Magufuli amelaani matukio yote ya kuwashambulia Askari Polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo.

Video: Makonda afanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa mabweni UDSM
Serikali yazidi kuwabana wakwepa kodi