Mgombea wa nne wa uchaguzi wa Rais unaotarajia kufanyika Desemba 20, 2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Delly Sesanga ametangaza kujiondoa na kumuunga mkono mfanyabiashara maarufu na Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi.
Hatua hiyo, inaimarisha umoja wa upinzani katika jitihada za kumshinda rais anayemaliza muda wake, Felix Tshisekedi wakilenga kurudisha utawala wenye kujali usalama wa raia na ulindaji wa rasilimali za Taifa hilo lenye utajiri wa Madini.
Sesanga ambaye ni Wakili na Mbunge wa Jimbo la Kasai ya Kati na Kiongozi wa Chama cha Envol, amesema nia yake ni kumuunga mkono Katumbi, mfanyabiashara tajiri akisema anastahili kuwaongoza wakongo.
Kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni mwezi uliopita, baadhi ya wagombea 26 walikuwa kwenye kinyang’anyiro hicho, lakini Waziri Mkuu wa zamani, Augustin Matata Ponyo na wagombea wawili ambao sio maarufu, walijiondoa na kumuunga mkono Katumbi.