Waziri wa Nchi (OR- Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo amesema kutungwa kwa sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022, kumefanikisha utoaji wa vivutio maalum kwa wawekezaji mahiri maalum (special strategic investors).
Prof. Mkumbo ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji Mahali Pamoja; Mwongozo wa Kuwasajili Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji pamoja na Kampeni ya Uhamasishaji Uwekezaji, jijini Dar es Salaam.
Amesema, “tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, tumeweza kutoa vivutio kwenye miradi mikubwa 16 ambayo inaendelea vizuri kikiwemo kiwanda cha kutengeneza vioo cha Mkuranga ambacho kilizinduliwa hivi majuzi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark Africa, Monica Hangi alisema amefurahi kushuhudia uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji kwani anaamini utasaidia kupunguza siku za maombi ya wawekezaji ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.
Ameongeza kuwa, “miaka miwili iliyopita, tulikuwa na mwekezaji ambaye alihitaji kutembea kwenye taasisi 12 ili apate vibali anavyostahili na aweze kuwekeza ndani ya nchi. Pia alihitaji kujaza fomu zaidi ya 50 kwa mkono, na akikosea kidogo anaanza upya. Hii ilikuwa inapoteza fursa nyingi na ilichosha wawekezaji.”