Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Nchini (DPP) Biswalo Mganga, amewafutia mashtaka na kuagiza kuachiwa huru mahabusu 147 waliokuwa wakisubiri kesi zao kutajwa mahakamani.
Akizungumza katika hafla maalumu ya uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ya wilayani Kahama, mkoani Biswalo amesema wamezingatia vigezo vikuu viwili vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ambavyo ni kuzingatia maslahi ya taifa na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha katika mashauri hayo.
“Wengine tumewafutia mashitaka kutokana ushahidi uliopo katika mashauri yao kutojitosheleza ambao utawezesha kuwatia hatiani pasipo kuacha shaka yeyote, pamoja na kuangalia maslahi ya taifa katika uendeshaji wa kesi hizo,”amesema Mganga.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Amoni Mpanju ameeleza kusikitishwa na uwepo wa washitakiwa wengi wa makosa ya mauaji yatokanayo na ramli chonganishi kutokana na migogoro ya kifamilia katika mikoa ya Shinyanga na Geita.
Aidha, Mpanju amewaagiza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha kila wanapojenga majengo ya umma kutenga vyumba viwili kwaajili ya Ofisi ya Taifa ya Mashitaka ili kurahisisha utendaji kazi na utoaji wa haki kwa wananchi.