Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezielekeza Halmashauri zote za Wilaya na Miji, kwenye maeneo yenye madini ziandae sheria ndogo (by-laws) kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya madini ili ziendane na Sheria ya madini.
Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza
Amesema, “wakurugenzi wa Halmashauri wekeni mifumo bora ya kuweka tozo hizo na kuondoa kero kwa wachimbaji wadogo, punguzeni utitiri wa tozo kwa kubuni vyanzo vingine mapato.”
Aidha, Waziri Mkuu pia amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuweka mazingira bora katika sekta ya uchimbaji mdogo na tayari imeshaanza kufanya marekebisho ya baadhi ya Kanuni na Sheria ya Madini na kuboresha mazingira ya biashara.
Kuhusu mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la Taifa, Majaliwa amesema umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017, hadi asilimia 7.2 mwaka 2021. “Pia katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta ya madini ni asilimia 9.6.”
Serikali kupitia sekta ya madini imeweza kukusanya shilingi bilioni 409.66 sawa na asilimia 85.43 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 479.51 katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023.