Beki wa Kulia Simba SC Shomari Salum Kapombe ametangaza uhakika wa kikosi cha Klabu hiyo kupambana vilivyo msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC ilimaliza msimu wa 2021/22 mikono mitupu, ikipoteza Ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ huku ikiishia hatua ya Robo Fainali katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwa kufungwa kwa changamoto ya Penati na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Kapombe amesema msimu uliopita ulikua mgumu kwa upande wao, lakini Simba SC imepanga kupambana msimu ujao ili kurejesha heshima yake iliyopotea.
“Msimu uliopita haukuwa mzuri kwetu, tulipoteza kila kitu, ilituumiza sana kwa kweli, lakini msimu ujao tutapambana ili kurejesha heshima yetu,”
“Tunamini timu yetu msimu ujao itakua Bora kwa sababu Uongozi umefahamu wapi tulipokosea, Mashabiki wanapaswa kuwa na imani na timu yao, kwa hakika hatutawaangusha.” Amesema Kapombe
Simba SC ilikua inatetea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya tano mfululizo, Kombe la Shirikisho mara ya tatu mfululizo, lakini mipango hiyo iliishia mikononi mwa watani zao wa jadi Young Africans ambao walifaidika na Ubingwa wa michuano hiyo kwa msimu wa 2021/22.