Ulimwengu mzima, hii leo Juni 14, 2023 unaadhimisha siku ya utoaji wa damu duniani huku Shirika la Afya duniani WHO, likiyahimiza mataifa yote ulimwenguni kuunga mkono shinikizo la kuwahimiza wananchi wao kujitokeza na kutoa damu kwa hiari.
Kwa mwaka huu siku hii inajikita na vijana na mchango wao katika kuokoa maisha kwa kujitolea damu. Kauli mbiu ikiwa “Toa damu na kuhakikisha dunia inaendelea kuishi”.
WHO na Taasisi zingine za afya zimelenga kutoa uelewa kwa watu juu ya umuhimu wa watu kujitolea damu mara kwa mara ili kuhakikisha upatikanaji wa damu safi na salama pamoja na vifaa vyake kwa ajili ya wagonjwa duniani kote.
Lakini barani Afrika katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara kiwango cha uchangiaji wa damu kimeshuka kwa asilim ia 17 tangu kuzuka kwa janga la Uviko-19 na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa katika huduma muhimu za afya maisha na uwezo wa watu kuishi.
Utoaji wa damu, husaidia kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kila mwaka kwani wagonjwa wanaougua na kuhatarisha maisha huokolewa na damu ambazo zipo katika benki ya kutunza Damu hasa wale wagonjwa wa dharula na wale wanaofanyiwa upasuaji wakiwemo wamama wanaotoka kujifungua.
Nchi nyingi zinakumbana na tatizo la upungufu wa damu katika benki za damu na tatizo la kupata damu safi na salama na ndio maana siku kuna haja wa watu kutambua juu ya umuhimu wa kuchangia damu safi na salama kwa ajili ya watu wengine waliopo mahospitalini wanaoteseka na tatizo la upungufu wa damu mwilini.
Tathmini ya WHO, imegundua kuwa mzunguko wa mwendo wa uchangiaji damu katika ukanda wa Afrika umepungua kwa asilimia 25 na mahitaji ya damu yamepungua kwa asilimia 13, na huku kukiwa na kusimamishwa kwa baadhi ya upasuaji wa kawaida katika nchi zingine na watu wachache wanaotafuta huduma katika vituo vya afya.
Katika siku hii ya utoaji damu duniani ni vyema watu wote wakaguswa na suala hili na kujitolea kutoa damu kwa hiari na kwa ajili ya kuwasaidia ndugu jamaa na marafiki wahitaji wenye upungufu wa damu, kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, anasema kusitishwa kwa usambazaji thabiti wa damu salama kunaweza kutishia maisha na anawashukuru watu kwa kuendelea kujitolea uchangiaji wa damu na kutaka nchi zianzishe na kuimarisha mifumo ya kuongeza michango ya damu ya hiari.