Benki ya Exim sambamba na wafanyakazi wa benki hiyo hii wiki hii walikabidhi msaada ya vyakula kwenye vituo vinne vya kulelea watoto yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Mjini Magharibi – visiwani Zanzibar.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaotekelezwa na benki hiyo unaofahamika kwa jina “Exim Cares”. Kwa mujibu wa uongozi wa Benki hiyo, msaada huo ulilenga katika kushiriki katika kuwapa faraha zaidi watoto hao hususan katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Eid.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Idara Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu. Akiwa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Malaika Kids, kilichopo wilayani Kinondoni, Kafu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza watoto wanaoishi kwenye vituo hivyo kusoma kwa bidii kwa kuwa taifa linategemea mchango wao katika kufanikisha maendeleo.
Msaada huo ulihusisha vyakula vya aina mbalimbali ikiwemo mchele, mafuta ya kupikia, sukari, maharage pamoja na vinywaji .
“Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kusherehekea Sikukuu ya Eid Ul Fitr, Benki ya Exim tuliona ni vema tusherehekee pamoja na watoto yatima pamoja na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia mahitaji haya muhimu ili na wao waweze kufurahia siku hiyo muhimu kama wenzao waliopo majumbani…tunashukuru wametupokea vizuri na wameonyesha kufurahishwa na hilo,’’ alisema.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mlezi wa kituo hicho Bi Neema Mohamed aliishukuru benki hiyo kwa wema huo huku akitoa wito kwa taasisi nyingine pamoja na watu binafsi kujitokeza pia ili kusaidia watoto wanaoishi kwenye vituo hivyo kwa kuwa mahitaji bado ni makubwa.
Angalia picha zaidi: