Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC Kipre Tchetche huenda akarejea Tanzania kufuatia kuhusishwa na mipango ya kusajiliwa na Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC.
Taarifa nyingine zinadai kuwa Azam FC pia wanajipanga kuingia kwenye vita ya kumrejesha nchini mshambuliaji huyo kutoka Ivory Coast, ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Malaysia.
Azam FC wamedhamiria kuboresha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe La Shirikisho (ASFC), huku Simba SC wakitarajia kufanya hivyo upande wa Kimataifa, baada ya kupata tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika.
Azam FC msimu huu imeshindwa kufurukuta katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kutetea taji la Kombe La Shirikisho (ASFC), baada ya kutolewa hatua ya Robo Fainali kwa kufungwa na Simba SC mabao mawili kwa sifuri.
Kabla ya kuchemsha Ligi Kuu na Kombe La Shirikisho, Azam FC walianza kulitema taji la Mapinduzi lililobebebwa na Mtibwa Sugar, mapema mwaka huu mjini Unguja, Zanzibar.
Endapo Tchetche atafanikiwa kujiunga na Azam FC ama Simba SC anatarajiwa kuwa na makali kama alivyokua kabla hajaondoka nchini miaka kadhaa iliyopita, kutokana na mazuri anayoyafanya hivi sasa kwenye ligi ya Malaysia.