Taarifa zinasema kuwa Uongozi wa Simba SC umeanza mazungumzo rasmi na Klabu ya Cotton Sports ya Cameroon kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa timu hiyo, Che Fondoh Malone ambaye anatajwa kuwa mrithi wa beki, Joash Onyango ambaye amewasilisha barua ya kutaka kuondoka klabuni hapo.
Hiyo ni katika kuelekea usajili wa dirisha kubwa litakalofunguliwa hivi karibuni baada ya msimu wa 2022/23 wa Ligi Kuu Bara kumalizika, huku Simba SC ikiwa tayari imeanza kufanya usajili wa kikosi chake, ikimsajili kiungo mshambuliaji wa Rayon Sports ya Rwanda, Willy Onana.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa, tayari mazungumzo kati ya uongozi wa Simba SC na wasimamizi wa mchezaji huyo (Royal Soccer Management) yameanza kwa ajili ya kumsajili.
Mtoa taarifa huzi amesema kuwa upo uwezekano wa beki huyo kujiunga na Simba SC kutokana na menejimenti ya mchezaji huyo kugomea baadhi ya ofa kadhaa ambazo wamepelekewa mezani.
Ameongeza kuwa kama mazungumzo yakienda vizuri, basi beki huyo atatua nchini hivi karibuni kwa ajili ya kukamilisha dili hilo la mkataba wa miaka miwili.
“Katika dirisha la usajili la mwezi Januari baadhi ya klabu zilionyesha nia ya kumuhitaji Malone, lakini yeye mwenyewe amegomea na kusimamia msimamo ya kuja kuichezea Simba SC.
“Hivi sasa mazungumzo yanakwenda vizuri, hivyo muda wowote atatua nchini kwa ajili ya kukamilisha dili la usajili katika kuelekea dirisha kubwa la usajili,” amesema mtoa taarifa huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu wa Simba Ahmed Ally akizungumzia masuala ya usajili ya timu hiyo, amesema: “Mazungumzo yanakwenda vizuri na baadhi ya wachezaji, mara baada ya usajili huo kukamilika kila kitu tutaweka wazi.”