Wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Simba SC, wanatarajiwa kurejea nchini kesho Jumanne (Desemba Mosi), wakitokea Nigeria ambako jana walicheza mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali, dhidi ya Plateau United.
Simba SC wameanza safari leo Jumatatu (Novemba 30) alfajiri kutoka mjini Jos hadi Abuja, mchana wataondoka Abuja kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo watafika usiku na kupumzika hapo.
Kikosi cha Simba SC kinatarajia kuwasili Tanzania kupitia Uwanja wa ndege wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) siku ya Jumanne, Desemba Mosi, saa 10:00 jioni.
Licha ya kuwekewa vikwazo vingi kwenye mchezo wa jana Jumapili (Novemba 29) wakiwa ugenini, kikosi cha Simba SC kilipambana na kupata matokeo ya bao moja kwa sifuri, hivyo kina kazi ya kufanya kwenye mchezo wa mkondo wa pili ili iweze kusonga mbele. Bao hilo pekee la Simba SC lilifungwa na Clatous Chama dakika ya 53.
Mchezo wa mkondo wa pili umepangwa kuchezwa Jumamosi (Desemba 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa.