Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamejinasibu kuwa makini kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons ambao watakua nyumbani mjini Sumbawanga mkoni Rukwa.
Simba waliwasili mjini humo jana wakitokea jijini Mbeya walipokua wameweka kambi ya siku mbili, huku wakiwa na morari kubwa ya kuhakikisha wanaendelea kufanya vyema kwenye michezo ya Ligi Kuu msimu huu.
Kufuatia umakini uliowekwa kuelekea mchezo huo, Uongozi wa klabu hiyo kongwe ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, umesema wamejipanga kupambana kikamilifu dhidi ya maafande hao wa Jeshi la Magereza, na wana matumaini ya kushinda.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Simba SC Haji Sunday Manara amesema, kikosi chao kipo tayari kwa mchezo huo, na tayari benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Sven Vanderbroek limekamilisha mikakati yake.
Hata hivyo Manara amesema pamoja na kuwa na matumaini ya kufanya vyema, bado wanawaheshimu wapinzani wao, kwa kutambua wana uwezo wa kupambana na kutoa upinzani wa dhati.
“Mchezo wetu wa Oktoba 22 dhidi ya Tanzania Prisons sio mwepesi kwani tunakutana na timu ngumu na yenye wachezaji wapambanaji muda wote. Unajua timu za majeshi zenyewe muda wote zipo fiti hapo unaweza kujua Simba tunakwenda kukutana na timu ya aina gani.”
“Kwa kuwa sisi ni mabingwa watetezi basi lazima tuingie kibingwa na tucheze tukiwa ni mabingwa watetezi, mashabiki wetu watupe sapoti ili timu ipate matokeo kwani tunahitai ushindi,” amesema Manara.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 13 sawa na Young Africans ambao wanazidiwa mabao ya kufunga, huku Azam FC wakiongoza msimamo huo kwa kufikisha alama 21.