Sakata la kikosi cha klabu ya Simba kuvaa jezi nyekundu ambazo zilionekana kushabihiana na zile za Stand United wakati wa mchezo wa mzunguuko wa tano wa ligi kuu ya soka Tanzania bara mwishoni mwa juma lililopita likiendelea kuwa gumzo, uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi umeomba radhi.
Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara ameulizwa juu ya suala hilo kuonekana kama liliwachanganya watazamaji hasa wa kwenye runinga, alisema wanaomba radhi kwa kilichotokea kwa kuwa kuna muingiliano wa mawasiliano ulitokea na hivyo kusababisha hali hiyo iwe hivyo.
Akifafanua zaidi Manara alisema, “kwanza tunaomba radhi kwa kilichotokea, sisi tuliokuwepo uwanjani tulikuwa hatuoni tatizo lolote, hata kwa mtu mwenye uwezo mdogo wa kuona au mwenye tatizo kidogo la kuona vizuri kama mimi niliweza kutambua utofauti uliokupo baina ya wachezaji wa Stand United na wale wa Simba.”
“Nimeambiwa kwenye TV (Azam TV) ndiyo ilikuwa na mkanganyiko kwa kuwa rangi za jezi zilionekana kufanana, hivyo halikuwa lengo letu kuwavuruga watazamaji,” aliongeza
Alipoulizwa sababu hasa ambayo ilisababisha tatizo hilo likatokea Manara hakuwa muwazi kufafanua zaidi ya kusema kuna tatizo la mawasiliano lililotokea.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, Simba ilipata ushindi wa mabao mawili kwa moja, lakini mfanano wa jezi ndio ulikua gumzo hasa kwenye mitandao ya kijamii.