Mabosi wa Simba SC wamegonga hodi kwa mara nyingine nchini Uganda, ili kuona kama wanaweza kumnasa kiungo mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC, Milton Karisa.
Karisa, ambaye kwa sasa yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda yenye mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Algeria utakaochezwa kesho Jumapili (Juni 18), amebakiza mkataba wa mwaka mmoja kwa mabingwa hao wa Uganda.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uganda, inaelezwa Kuwa Simba SC imeonyesha nia ya kumsajili nyota huyo ambaye alikuwa sehemu ya mafanikio ya Robertinho, wakati akiinoa timu hiyo, hata hivyo Wekundu wa Msimbazi wanakabiliwa na upinzani kwenye dili hilo kutoka kwa APR ya Rwanda.
Siku chache zilizopita, Robertinho alisema kazi yake kuhusu usajili ilimalizika wakati ambao alikabidhi ripoti na mapendekezo yake, kilichobaki ni utekelezaji ili kukibore sha kikosi chao.
“Nina matumaini makubwa na msimu ujao, tumepanga mambo mengi mazuri ikiwemo kuwa na maandalizi mazuri nataka kusaka kikosi bora zaidi cha ushindani ambao utarejesha furaha kwa mashabiki wetu,” alisema.
Mwaka 2016 ambao Karisa alianza kuichezea Vipers kabla ya kuondoka na kisha kurudi tena 2020, ameisaidia timu hiyo kutetea ubingwa msimu huu 2022/23.